MISINGI KIROHO
TENGENEZA MISINGI YAKO ILI UWEZE KUZIONA BARAKA ULIZOWEKEWA NA MUNGU MBELE YAKO.
3 Kama misingi ikiharibika, Mwenye haki atafanya nini? (ZABURI.11:3)
SEHEMU YA KWANZA.
CHANZO CHA KUHARIBIKA KWA MISINGI YA MWENYE HAKI NI NINI?
1.NINI MAANA YA MISINGI?
Msingi ni kitu ambacho kinachobeba kitu kingine au ni mtaji ambao husababisha uzalishaji wa aina fulani, katika lugha lahisi zaidi ambayo huenda ikaeleweka na watu wengi msingi ni miguu ya kusimamia, tunaelewa ili mwanadamu aweze kusimama anaitaji awe na miguu na ili akimbie anaitaji awe na miguu, na pia ili aweza kutembea anaitaji kuwa na miguu. Hapo najaribu kukufungua ufahamu wako juu ya msingi.
Pengine kwa tafsiri nyingine tunaweza kusema kwamba misingi ni vyanzo katika jambo lolote, nimejaribu kutafuta sana kwa kila jambo kuna vyanzo na hivyo vyanzo ndiyo misingi maana hakuna jambo lisilo kuwa na msingi wake hata dunia tu ina misingi kama tusomavyo;
Tuone Mungu alipokuwa anamjibu Ayubu alimwuliza juu ya uumbaji wake akasema;4 Ulikuwa wapi nilipoiweka misingi ya nchi? Haya!Sema kama ukiwa na ufahamu.
(AYUBU.38:4); 10 Na tena, Wewe,Bwana,hapo mwanzo uliitia misingi ya nchi, Na mbingu ni kazi za mikono yako.(WAEBRANIA.1:9) Nchi maana yake ni ardhi yenye mipaka halali ya kiumiliki.
Kwa hiyo ardhi uliopo ina misingi yake na hiyo misingi ni kwa ajili ya kuibeba hiyo ardhi yako, na ikiwa misingi yake ikiharibika utapata shida sana. Kwa hiyo tumepata kuona kuwa kila jambo lina misingi yake ya kulifanya liweze kusimama katika ulimwengu wa kiroho; angalia
• Hutumishi wa mtu una msingi wake,
• Ndoa ya mtu ina misingi yake,
• Afya ina misingi yake,
• Biashara ina misingi yake,
• Elimu yako ina misingi yake,
• Uzao wako una misingi yake,
• Mafanikio ya mtu yana misingi yake, n.k
Hapo tumeona baadhi ya misingi ya mtu, kwamba hivyo ulivyo kuna misingi iliokushikiria na kama misingi yako imeharibika hujue maisha yako utakuwa ni mtu wa kutanga tanga huna makao maalum; afya haina makao, ndoa haina makao, biashara haina makao. Ukianza kuona uharibifu katika nafasi yako angalia misingi yako imekaaje, viwango vyako vya kiroho vikoje?
2.NINI MAANA YA MWENYE HAKI?
HAKI:Maana yake ni jambo lililolako kihalali kufuatana na sheria na hukumu za Mungu kama hakimu au mwamuzi mwenye haki. Mungu ni hakimu mwenye Haki kwa sababu hukumu zake ni za haki, za halali, hana upendeleo anakulipa sawasawa na haki yako.
Tuone neno la Mungu linavyosema; 34 Petro akafumbua kinywa chake, akasema, Hakika natambua ya kuwa Mungu hana upendeleo;
35 bali katika kila taifa mtu amchaye na kutenda haki hukubaliwa na yeye. (MATENDO YA MITUME.10:34-35)
Kwa hiyo kwa ufupi tafsiri ya mwenye haki ni mtu wa Mungu, ni mtakatifu, aliyetengwa kwa ajili ya utukufu wa Mungu. Na hao ni wakristo waliotengwa na huu ulimwengu wa maovu kwa ajili ya utukufu wa Mungu hapa duniani na maisha baada ya kifo huko mbinguni.
3.CHANZO CHA KUHARIBIKA KWA MISINGI YA MWENYE HAKI.
Mungu alipomwumba mwanadamu, mwanadamu alikuwa ni mwenye haki, alikuwa na haki zote za kimungu zilizokuwa upande wake huyo mwanadamu kwa mfano;
• Uzima wa milele ni haki ya Mungu ilikuwa ndani ya mtu,
• Kukaa na Mungu ilikuwa ni haki yake,
• Kuangaliwa na Mungu ilikuwa ni haki yake,
• Kusikilizwa na Mungu ilikuwa ni haki yake,
• Kuishi bila mateso ya umaskini na magonjwa ilikuwa ni haki yake,
• Kulindwa na Mungu pamoja na haki nyingi mbalimbali za Mungu zilikuwa ndani ya huyo mwanadamu.
Lakini mwanadamu alipotenda dhambi misingi yake ikaharibika, akapoteza haki zake zote, akawa mateka kwa ibilisi Mungu akajitenga nae kwa hiyo akaondolewa kuitwa mwenye haki kwa sababu haki zake amezipoteza.Mwanadamu alikuwa ni mwenye haki hapo kwanza alipokuwa hajatenda dhambi.
DHAMBI NI NINI?
DHAMBI:Ni uasi. Na uasi ni kwenda kinyume na maagizo au kwenda kinyume na sheria au kwenda kinyume na maelekezo, kama tusomavyo;
4 Kila atendaye dhambi, afanya uasi; kwa kuwa dhambi ni uasi. (1 YOHANA.3:4)
Na dhambi ina madhara ya umauti katika eneo inalokuwepo, Biblia inasema 23 Kwa maana mshahara wa dhambi ni mauti; bali karama ya Mungu ni uzima wa milele katika Kristo Yesu Bwana wetu. (WARUMI.6:23)
Angalia viwango vyako vya kiroho vikoje, na misingi yako ikoje, je, hakuna umauti? Ukiona umauti katika nafasi yoyote yoyote inayokuhusu kuna dhambi ilioingia ndani, kuna maasi yaliofanyika. Mwanadamu alipoumbwa na kuwekwa bustani ya Edeni alipewa maagizo, na agizo la kwanza alilopewa ni kuzaa na kuijaza nchi, kuitiisha na kutawala, ukisoma kitabu cha Mwanzo tunaelekezwa habari hizo;
27 Mungu akaumba mtu kwa mfano wake, kwa mfano wa Mungu alimwumba, mwanamume na mwanamke aliwaumba.
28 Mungu akawabarikia, Mungu akawaambia, Zaeni, mkaongezeke, mkaijaze nchi, na kuitiisha; mkatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na kila kiumbe chenye uhai kiendacho juu ya nchi. (MWANZO.1:27-28)
Tuone Biblia inavyosema, Mungu akawaambia, Zaeni, mkaongezeke, mkaijaze nchi.. Neno AKAWAMBIA Hili ni agizo/amri/sheria anawaamru nini? ZAENI, MKAONGEZEKE, MKAIJAZE NCHI NA KUITISHA; MKATAWALE haya ni maagizo au ni sheria kwao kuitimiza, kuitii na kuifuata.
Kwa hiyo ukiona wewe ni tasa havizaliwi vitu kwako, huna maono ya kuzaa vitu, ujue moja misingi yako imeharibika sio mpango wa Mungu mwanadamu asizae vitu katika ulimwengu wa roho na kimwili!
Pia lingekuwa jambo la ajabu kama mbwa ingeaanza kumtawala mwanadamu sio mpango wa Mungu wanyama kumtawala mwanadamu ndiyo maana unaona kwa uwezo huo wanyama wanatutii tunawakusanya na kuwaweka kwenye mbuga ni mpango wa Mungu ndiyo msingi tuliowekewa wa kuwatawala, pia mpango wa Mungu kwa mwanadamu msingi aliokuwa amemwekea ni ili aongezeke awe na utele katika ulimwengu wa kiroho na hata katika dunia.
Sasa ukiona ulikuwa una utele ghafula ukaanza kuona mambo yako yanafifia, unaanza kubaki na stori nilikuwa na jambo fulani,ooh! Nilikuwa na gari, kiwanja, nyumba, mke/mme mzuri, mshahara mzuri huo sio mpango wa Mungu misingi yako imeishaharibika hata kama unajifariji hamna kitu!
Tumeona misingi ya mwenye haki ilikuwa ni kuzaa vitu katika ulimwengu wa kiroho na mwilini, kuongezeka, kumiliki na kutawala ilikuwa ni haki yake. Hiyo ndiyo misingi ya mwenye haki aliokuwa amewekewa mwenye haki hapa duniani tangu mwanzo.
Na haki yake na misingi yake huyu mwenye haki ingeweza kudumu kwake kama angedumu katika kutii neno la Mungu tunasoma jinsi Mungu alivyomwonya na kumpa maelekezo ya kuidumisha hiyo haki yake kwake;
15 Bwana Mungu akamtwaa huyo mtu, akamweka katika bustani ya Edeni, ailime na kuitunza.
16 Bwana Mungu akamwagiza huyo mtu, akisema, Matunda ya kila mti wa bustani waweza kula,
17 walakini matunda ya mti wa ujuzi wa mema na mabaya usile, kwa maana siku utakapokula matunda ya mti huo utakufa hakika. (MWANZO.2:15-17)
Na pia hili lilikuwa ni agizo lingine katika bustani ya Edeni; kuilima bustani na kuitunza, na kujiepusha na liletunda la mti wa ujuzi wa mema na mabaya. Mpango wa Mungu anataka huitunze ardhi yako, mpango wa Mungu tusiharibu lakini kwa kutotii neno la Mungu mwanadamu aliasi. Uasi ni dhambi. 4 Kila atendaye dhambi, afanya uasi; kwa kuwa dhambi ni uasi. (1YOHANA.3:4)
Kwa hiyo mwanadamu akamwasi Mungu kwa kutotii neno la Mungu akachukua tunda aliloamriwa asile yeye akala kama tusomavyo; 6 Mwanamke alipoona ya kuwa ule mti wafaa kwa chakula, wapendeza macho, nao ni mti wa kutamanika kwa maarifa, basi alitwaa katika matunda yake akala, akampa na mumewe, naye akala. (MWANZO.3:6)
,
Dhambi hii ya kutolitii neno la Mungu ikamfanya mwenye haki misingi yake iharibike apate umauti katika nafasi yake na kuwa mbali na Mungu. Kwa hiyo chanzo cha misingi ya mtu kuharibika ni dhambi na dhambi imebeba mauti kwa muhusika. Mpendwa misingi yako imesimamaje?
viwango vyako vya kiroho vikoje maana dhambi ndiyo chanzo cha misingi ya mwenye haki kuharibika.
15 Lakini karama ile haikuwa kama lile kosa; kwa maana ikiwa kwa kukosa kwake yule mmoja wengi walikufa, zaidi sana neema ya Mungu, na kipawa kilicho katika neema yake mwanadamu mmoja Yesu Kristo kimezidi kwa ajili ya wale wengi.
16 Wala kadiri ya yule mtu mmoja aliyefanya dhambi si kadiri ya kile kipawa; kwa maana hukumu ilikuja kwa njia ya mtu mmoja ikaleta adhabu; bali karama ya neema ilikuja kwa ajili ya makosa mengi, ikaleta kuhesabiwa haki.
17 Kwa maana ikiwa kwa kukosa mtu mmoja mauti ilitawala kwa sababu ya yule mmoja, zaidi sana wao wapokeao wingi wa neema, na kile kipawa cha haki, watatawala katika uzima kwa yule mmoja, Yesu Kristo.
18 Basi tena, kama kwa kosa moja watu wote walihukumiwa adhabu, kadhalika kwa tendo moja la haki watu wote walihesabiwa haki yenye uzima.
19 Kwa sababu kama kwa kuasi kwake mtu mmoja watu wengi waliingizwa katika hali ya wenye dhambi, kadhalika kwa kutii kwake mmoja watu wengi wameingizwa katika hali ya wenye haki.
20 Lakini sheria iliingia ili kosa lile liwe kubwa sana; na dhambi ilipozidi, neema ilikuwa nyingi zaidi;
21 ili kwamba, kama vile dhambi ilivyotawala katika mauti, vivyo hivyo kwa njia ya haki neema itawale hata uzima wa milele kwa Yesu Kristo Bwana wetu. (WARUMI.5:15-21)
Nakushukuru kwa kufuatana na mimi katika mwanzo somo letu, nikuombe twendelee kumwomba Mungu ikimpendeza tupate neeme twendelee na sehemu ya pili. Mpendwa natamani somo hili lifanyike baraka kwako pale misingi yako ilipokuwa imeharibika ukamgeukie Yesu Kristo leo na misingi yako ipate kuhimarishwa tena, hayo maisha ya uovu na mateso sio mpango wa Mungu kwako haki zetu ziliibiwa na ibilisi walakini Yesu Kristo amekuja kurejesha haki tulizokuwa tumepoteza
UBARIKIWE SANA SANAA
Mobile phone: 0769894137-whatsaap
0788650274- Call
Na Mwl. Timothy Sangayoni.

No comments